Kutoa vibali vya hitimisho la kazi kwa Walimu

MASUALA YA HITIMISHO LA KAZI YA WALIMU.

Kanuni ya 9 (1) (a)-(g) ya Kanuni za Utumishi wa Walimu za mwaka 2016, imefafanua mambo ambayo yanaweza kumsababishia Mwalimu ahitimishe kazi ya Ualimu.  Mambo hayo ni pamoja na kustaafu kwa kutimiza umri kwa mujibu wa Sheria (kustaafu kwa hiari na kwa lazima), kustaafu kwa ugonjwa, kuachishwa kazi kwa masuala ya kinidhamu, kufariki, kuacha kazi kwa hiari, kustaafishwa kwa manufaa ya Umma, kufutwa kwa Ofisi na kugombea nafasi za Uongozi / kisiasa.

Aidha, kwa mujibu wa Waraka wa Katibu Mkuu UTUMISHI wenye Kumb. Na. CB.45/254/02/1 wa tarehe 11/08/2004 Kifungu cha 4. Mamlaka za Ajira na Nidhamu zimepewa jukumu la kutoa vibali vya kustaafu kwa watumishi wake wanapostaafu.

Utaratibu utakaotumika Mwalimu anapohitimisha utumishi kwa kustaafu kwa lazima au hiari

  1. Ofisi za Tume ngazi ya Wilaya zitaandaa maoteo ya kustaafu kazi walimu ya kipindi cha miaka mitano na kuwasilisha nakala Tume Makao makuu na kwa Mwajiri;
  2. Ofisi za Tume Wilayani zitawajulisha walimu wanaostaafu kazi kwa lazima miezi sita kabla ya kustaafu kwao ili kuepuka kupitiliza muda wa kustaafu;
  3. Katibu Msaidizi wa Tume ngazi ya Wilaya ataandika kibali cha kustaafu kazi na kibali hicho kitapitishwa na Mwajiri kabla ya kukabidhiwa kwa Mwalimu husika.
  4. Ofisi za Tume Wilaya zinatunza kumbukumbu zote muhimu za kiutumishi za Walimu wanaostaafu.

         

Umri wa kustaafu kwa Hiari na kwa Lazima.

 1. Kustaafu kwa lazima na kwa hiari kunategemea tarehe ya kuzaliwa kwa mwalimu. Mwalimu anaruhusiwa kustaafu kwa hiari afikishapo umri wa miaka 55 na atalazimika kustaafu kwa lazima afikishapo umri wa miaka 60. Tarehe ya kuzaliwa Mwalimu itakayozingatiwa ni ile aliyoijaza kwenye kumbukumbu zake za kiutumishi alipoanza kazi ‘’History Sheet’’.
 2. Endapo itatokea kwenye kumbukumbu za kuzaliwa Mwalimu alijaza mwaka bila tarehe, tarehe yake itakuwa 1 Julai ya mwaka atakaostaafu. Aidha, ikitokea kuwa alijaza mwezi na mwaka bila tarehe, tarehe yake ya kuzaliwa itakuwa tarehe 15 au 16 ya mwezi huo;
  1. Endapo kutakuwa na mgongano wa tarehe ya kuzaliwa kwenye kumbukumbu zake za kiutumishi tarehe itakayotambuliwa kuwa ni tarehe yake sahihi ya kuzaliwa ni ile inayompa umri mkubwa chini ya kisahihisho cha Kifungu F.47 (1 - 2) cha Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009.

 Utaratibu wa kustaafu kazi kwa Ugonjwa

Utaratibu wa kustaafu kazi kwa ugonjwa umeainishwa kwenye Kanuni ya 30 (1)  na 100 (1) - (2) za Kanuni za Tume ya Utumishi wa Umma, 2003 Mtumishi yeyote katika kutekeleza majukumu yake anaweza kupata matatizo ya afya yatakayomfanya kushindwa kutekeleza majukumu yake. Mamlaka ya Ajira itafanya mchakato wa kumstaafisha mtumishi atakapothibitishwa na daktari kushindwa kutekeleza majukumu yake kutokana na sababu za ugonjwa; Utaratibu utakaotumika ni kama ufuatavyo: -

 1. Mtumishi atakayekuwa na matatizo hayo ya kiafya atalazimika kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu. Mtumishi atapewa likizo ya Ugonjwa kwa miezi isiyozidi sita, likizo hiyo itakuwa ya malipo ya mshahara kamili. Iwapo Mtumishi atakuwa bado hawezi kutekeleza majukumu ataongezewa muda wa likizo ya ugonjwa kwa miezi sita mingine na kulipwa nusu mshahara katika kipindi chote. Endapo mtumishi/mgonjwa hatapata nafuu (kupona) kwa kipindi hicho, mapendekezo ya kumstaafisha kwa sababu za ugonjwa yatatolewa, kwa: -.
 2.  Mamlaka ya Ajira italazimika kuunda jopo la Madaktari ili kuchunguza afya ya mtumishi na kushauri iwapo mtumishi anaweza kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kazi au astaafishwe kwa ugonjwa.
 3. Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na Jopo la Madaktari/ Mganga Mkuu atawasilisha taarifa ya uchunguzi pamoja na mapendekezo kwa Mamlaka ya Ajira.
 4. Kamati ya Wilaya itapokea taarifa na kutoa uamuzi kulingana na mapendekezo ya jopo. Uamuzi utakaotolewa na Mamlaka ya Ajira nakala atapewa Katibu Mkuu - UTUMISHI.
 5. Mwalimu atastaafishwa kwa ugonjwa tangu tarehe ambayo Mamlaka ya Ajira ilipokea taarifa na mapendekezo kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

8.1.3 Utaratibu wa kuacha kazi

Kanuni ya F.49 ya Kanuni za kudumu za Utumishi wa Umma imefafanua utaratibu wa kuacha kazi Mtumishi wa umma ikiwa ni pamoja na Mwalimu anaweza kuacha kazi ya ualimu muda wowote kwa kufuata utaratibu ufuatao: -

 1. Kumtaarifu mwajiri uamuzi wake wa kuacha kazi kwa kuandika barua ndani ya saa 24
 2. Kurudisha mshahara wa mwezi mmoja kwa Mwajiri wake na vifaa vyote alivyokuwa anatumia katika kipindi cha utumishi wake
 3. Mtumishi atapewa cheti cha kuondoka katika utumishi wa Umma na Mwajiri.
 4. Aidha, mtumishi ambaye yupo kwenye kipindi cha uangalizi (probation period) ataacha kazi ndani ya kipindi cha miezi mitatu ya uangalizi naye pia anapaswa kuandika barua kwa mwajiri juu ya nia yake ya kuacha kazi ndani ya kipindi hicho. Ataendelea na kazi hadi muda utakapofika atakabidhi vifaa na majukumu aliyokuwa nayo.

          Utaratibu wa kuhitimisha kwa kugombea nafasi za kisiasa

Utaratibu wa kuhitimisha utumishi wa umma kwa kugombea nafasi za kisiasa umeanishwa kwenye Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Na. 1 wa tarehe 2.1.2015 unaohusu utaratibu kwa watumishi wa umma wanaogombea nyadhifa za kisiasa nchini. Waraka huo umefafanua utaratibu wa watumishi wote wa umma wenye nia ya kugombea nyadhifa za kisiasa kama ifuatavyo: -

 1. Mtumishi wa umma atakayeamua kugombea nafasi ya ubunge wa kuchaguliwa, viti maalumu vya ubunge au nyadhifa nyingine za kisiasa ataruhusiwa kufanya hivyo, baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza kuwa mgombea wa ubunge atalazimika kuacha kazi na kulipwa mafao yake
 2. Mtumishi wa Umma anayeteuliwa na Rais kuwa Mbunge, atakuwa na hiari ya kuchukua likizo bila malipo kwa kipindi chote atakachokuwa Mbunge, au kuacha kazi na kulipwa mafao yake kuanzia siku atakayoteuliwa kuwa Mbunge.
 3. Endapo mtumishi atashindwa katika uchaguzi na akataka kurejea kwenye utumishi wa umma, atalazimika kuomba ajira upya kwa Mamlaka zinazohusika.
 4. Kwa mtumishi atakayechukua likizo bila malipo akimaliza likizo hiyo ya kipindi cha uteuzi kurejea kwake kazini kutategemea kuwepo kwa nafasi ya kumwajiri katika utumishi wa umma.
 5. Iwapo mtumishi atasita kupokea uteuzi wa Rais au wa Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ataruhusiwa kuendelea kuwa mtumishi wa umma.

Utaratibu wa kuhitimisha kwa kufukuzwa kazi

Mtumishi wa Umma anaweza kuhitimisha utumishi wake kwa kufukuzwa kazi baada ya kukiuka Sheria, Kanuni na Taratibu zinazoongoza utumishi wa umma.

Mwalimu akithibitika kuwa amefanya jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya utumishi wa walimu/umma, atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu Na. 25 ya mwaka 2015 na Kanuni zake za mwaka 2016. Ikithibitika kosa alilotenda linaangukia kwenye makosa mazito/makubwa adhabu anazoweza kupewa ni pamoja na kufukuzwa kazi na hivyo kuhitimisha utumishi wake. Aidha, Mwalimu kama ilivyo kwa watumishi wengine wa Umma akithibitika kuwa amefanya jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya utumishi wa umma, kupitia taarifa zilizowasilishwa na Mamlaka mbalimbali anaweza kustaafishwa kwa manufaa ya Umma baada ya Rais kuridhia kutolewa kwa adhabu hiyo. Mtumishi atapoteza haki zake zote. Hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 29 (1) – (3) ya Kanuni za Tume ya Utumishi wa Umma, 2003 na Kanuni ya F.40(1) ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, 2009.

                                          Kufariki

Utumishi wa Mwalimu kama ilivyo kwa watumishi wengine wa Umma utakoma baada ya mwalimu huyo kufariki.