TSC KUTUMIA SHILINGI BILIONI 20.74 MWAKA UJAO WA FEDHA

19 Apr, 2024
TSC KUTUMIA SHILINGI BILIONI 20.74 MWAKA UJAO WA FEDHA

Tume ya Utumishi wa Walimu imepanga kutumia shilingi bilioni 20.74 katika mwaka wa fedha wa 2024/25 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo katika kuwahudumia walimu.

Kauli hiyo imetolewa tarehe 16 Aprili, 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI  kwa Mwaka wa Fedha 2024/25.

Alisema fedha hizo zitatumika kusimamia ajira na maendeleo ya walimu kwa kuhakikisha kwamba walimu wanasajiliwa, wanathibitishwa kazini na kwa wale wenye sifa wanapandishwa vyeo na kubadilishiwa kada kwa wakati.

Mhe. Mchengerwa aliongeza eneo jingine ambalo fedha hizo zitatumika ni kusimamia maadili na nidhamu kwa walimu wa shule za msingi na sekondari katika utumishi wa umma ili watekeleleza wajibu wao wa kufundisha wanafunzi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu na Utumishi wa Umma.

Pia, aliongeza kuwa fedha hizo zitasaidia katika kufanya utafiti na kutathmini hali ya walimu nchini na kubainisha aina na mahitaji ya walimu, idadi na ngazi ya walimu wanaohitajika.

Mhe. Mchengerwa alisema Tume itaendelea kukamilisha utengenezaji wa Mfumo wa Teachers’ Service Commission Management Information System (TSCMIS), usimikaji wa miundombinu ya mtandao wa intaneti katika Ofisi 115 za Wilaya na kuendelea na ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tume Makao Makuu jijini Dodoma.