Walimu katika Utumishi wa Umma wamegawanyika katika kada/ makundi makuu matatu kama yalivyoainishwa katika Waraka Na. 1 wa mwaka 2014 unaohusu Miundo ya Utumishi wa Kada za Walimu. Makundi hayo ni:-
i) Walimu Daraja A – hawa ni Walimu wa ngazi ya Cheti;
ii) Walimu Daraja B – hawa ni Walimu wa ngazi ya Stashahada na;
iii) Walimu Daraja C – hawa ni Walimu wa ngazi ya Shahada.
1. Kuwabadilishia cheo Walimu
Mwalimu anapojiendeleza kutoka ngazi moja ya Elimu kwenda ngazi nyingine atatakiwa kubadilishiwa cheo kwa kuzingatia Waraka wa Katibu Mkuu UTUMISHI Na. 1 wa Mwaka 2014 unaohusu Miundo ya Utumishi wa kada za Walimu sambamba na Waraka wa Utumishi Na. 1 wa Mwaka 2011 wenye Kumb. Na. CAC.44/45/01/A/121 wa tarehe 20, Desemba 2011 kuhusu utaratibu wa kuwabadilishia Kazi/Cheo Walimu waliojiendeleza.
2. Mambo muhimu ya kuzingatiwa katika kuwabadilishia Kazi /cheo Walimu
i) Mwalimu husika ataandika barua ya kuomba kubadilishiwa cheo ikiwa imeambatishwa nakala ya Cheti cha kuhitimu mafunzo kwa ngazi husika (Stashahada / Shahada). Barua hiyo itawasilishwa kwa Katibu Msaidizi wa Wilaya kupitia kwa Mwajiri wake;
ii) Mwalimu aliyejiendeleza kielimu atabadilishiwa Cheo/Kazi kwa kuzingatia ngazi ya mshahara (Horizontal). Mfano, Mwalimu Daraja IA ngazi ya mshahara TGTS D mwenye Astashahada atabadilishwa kuwa Mwalimu Daraja la II B ngazi ya mshahara TGTS D akijiendeleza kwa ngazi ya Stashahada au atabadilishwa kuwa Mwalimu Daraja la III C ngazi ya mshahara TGTS D akijiendeleza kwa ngazi ya Shahada.
iii) Mwalimu atabadilishiwa Kazi/Cheo baada ya kuwekwa kwenye Ikama katika mwaka wa fedha husika bila kujali kuwa kubadilishwa huko kutakuwa/hakutakuwa na athari katika mshahara wake kwa kuwa cheo atakachokuwa nacho baada ya kubadilishiwa ni cheo tofauti na cheo alichokuwanacho awali. ( Job Code tofauti)
iv) Mwalimu anapobadilishiwa kazi / cheo baada ya kujiendeleza, cheo anachokuwa nacho wakati huo kitahesabika kuwa ni cheo kipya, na hivyo kwa mujibu wa ufafanuzi uliotolewa na Katibu Mkuu (UTUMISHI kwa barua Kumb. Na. CAC.45/257/01/E/83 ya tarehe 9.9.2013 ), atapaswa kutumikia cheo hicho kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu kabla ya kufikiriwa kupandishwa cheo kingine. Hii ni katika kulinda ukubwa (Seniority) kwa walimu waliopata sifa awali katika kada husika ikilinganishwa na wale wanaopata sifa hizo baadaye. Mfano Mwalimu aliyeanza kazi Mwaka 2010 akiwa na Shahada (MD IIIC, ngazi ya Mshahara TGTS D) ikichukuliwa kuwa alipandishwa vyeo kila baada ya miaka mitatu (Ukiondoa mwaka mmoja wa matazamio), mwaka 2018 atapandishwa na kuwa MD IC ngazi ya mshahara TGTS F. Cheo hicho kitakuwa sawa na cheo cha mwalimu wa Astashahada ambaye alipandishwa vyeo kwenye kada yake na kufikia cheo cha Mwalimu Mwandamizi B, ngazi ya mshahara TGTS F. Mwalimu huyu kwa mfano akiwa amejiendeleza kwa ngazi ya Shahada na kuhitimu mwaka 2018 na akabadilishiwa cheo atakuwa na Cheo cha MD I, TGTS F. Tafsiri yake ni kuwa Mwalimu aliyeanza kazi mwaka 2010 akiwa na shahada atakuwa analingana cheo na mwalimu aliyepata sifa hiyo miaka 8 baadaye.
3. Uhusiano uliopo kati ya Kubadilishiwa Kazi / Cheo na Kupandishwa cheo Mwalimu aliyejiendeleza.
i) Mwalimu aliye masomoni kwa muda mrefu hataweza kupandishwa cheo kwa wakati huo kwani kupandishwa cheo ni kupewa tuzo kutokana na utendaji kazi mzuri. Mwalimu aliye masomoni hatekelezi majukumu ya kazi yake;
ii) Mwalimu aliyebadilishwa Kazi/Cheo atatakiwa kutumikia Cheo hicho kwa muda usiopungua miaka mitatu au zaidi kadri ya maelekezo yatakavyokuwa yakitolewa kabla ya kupandishwa kwa kuwa mwalimu huyo atakuwa ameingia kwenye kundi lenye cheo tofauti na kundi alilotoka hata kama mshahara utabaki kuwa ule ule. Hivyo, atawakuta Walimu waliokuwa kwenye kundi hilo jipya kabla yake.
Mwalimu hataweza kubadilishwa na kupanda cheo hapo hapo na kuonekana kwamba ameingia kwenye kundi muda mrefu na kuwaacha/kuwazidi aliowakuta tayari kwenye kundi hilo walio kwenye ngazi ile ya mshahara.
Secretary PO-TSC
Postal Address: P. o Box 353 DODOMA
Telephone: +255 26 2322402
Mobile:
Email: secretary@tsc.go.tz
Copyright ©2017 TSC . All rights reserved.